• NEWS & SPORTS

    TANZANIA MPYA

    Sunday, February 19, 2017

    Maalim Seif Amtolea 'Povu' Prof Lipumba na Makundi Yake,Amchana Hadharani Juu ya Fitina Wanazofanya Cuf



    KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewafunda wafuasi wake na kuwataka kuepuka fitna ambazo zitasababisha kukigawa chama chao.
    Maalim Seif aliyaeleza hayo katika Kijiji cha Matele Jimbo la Chambani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba alipoweka jiwe la msingi la tawi la chama hicho.
    Alieleza kuwa wapo baadhi ya watu waliokuwa wabunge wa chama hicho, lakini baada ya kukataliwa na wanachama majimboni kwa sasa wamenuna na kuanzisha migogoro ndani ya chama hicho.
    “Walidhani vile vyeo ni mali yao, sasa wamesahau kuwa wenye mamlaka ya kuteua mgombea ni wanachama, wanaanza kutaka kuharibu, lakini waambieni watajiharibu wenyewe na siyo chama hiki,” alieleza Maalim Seif.
    Aliwaambia wanachama hao kuwa wakati huu ni vyema wakawa na umoja na kufanya kazi kwa pamoja katika chama ili kufikia malengo waliojiwekea.
    “Wako watu wanajiita Mungiki, ambao wana nia mbaya na chama hiki, lakini tunawaambia nia zao zitawarejea wenyewe,” alieleza Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
    Alieleza kuwa kila mnafiki katika chama hicho atadhihirika na atatoka na kukiacha chama kikiendelea.
    “Kwa hiyo ili kuwadhibiti hawa, ni vyema tukazidisha umadhubuti wa umoja wetu na kuwafagia wote ili chama kizidi kuwatia joto CCM na Seriklai zake,” alisema.
    Alisema kuna watu kwa tamaa zao wamekubali kupokea hongo na kuanza kukihujumu chama chao huku akisema kuwa wamechelewa.
    Maalim Seif alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa siku nyingi wamekuwa wakikiandama CUF kutokana na kuwa malengo ya kuwakomboa Wazanzibar na Watanzania, lakini wameshindwa kutokana na uimara walionao.
    Aidha, alisema kuwa CCM wakiona chama cha upinzani kina dalili ya kuwaondoa madarakani, wanakifanyia kila aina ya hujuma ili kukimaliza na kudai kuwa hawana tena nguvu hiyo dhidi ya CUF.
    “Wanatia migogoro katika vyama vya upinzani na kuwahujumu viongozi wake baada ya kuona wakati wowote madaraka yatawatoka,” alisema.
    Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Salim Biman, alielza kuwa wasaliti wote ambao wamekisaliti chama hicho ni wale aliodai hawakuwa na machungu ya kuwakomboa Watanzania ambao tayari wameshachagua mabadiliko.
    Aliwataka wanachama hao kutowapa nafasi wale aliodai mamluki kwani hawana nia nzuri kwa chama chao.
    “Huu msukosuko unaopita kwenye chama chetu akipenda Mwenyezi Mungu utakwisha, licha ya kupata baraka za SMZ na SMT,” alieleza Biman.
    Wakati huo huo Maalim Seif alizindua magari maalum kwa ajili ya kutoa huduma kwa Jimbo la Chambani ambayo yalitolewa na Mbunge wa jimbo hilo, Yusouf Salim Husein.

    No comments: