Serikali imetangaza orodha ya wanafunzi ambao watarejea kuendelea na
masomo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) baada ya uchambuzi kumalizika
na kupatikana idadi ya wanafunzi ambao wana sifa za kuendelea na
masomo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema kuwa kwa kipindi chote
walikuwa wakifanya uchambuzi ili kuona ni wanafunzi gani walikuwa na
sifa za kusoma kozi hiyo maalum ambayo ilianzishwa kutokana na tatizo la
walimu wa Sayansi.
Alisema kuwa programu hiyo ilikuwa inahitaji walimu ambao watakwenda
kufundisha shule za sekondari lakini kulikuwa na wanafunzi 1,210 ambao
walikuwa wanachukua stashahada ya ualimu wa shule za msingi ambao ni
kinyume na malengo na 6,595 wakichukua stashahada ya kufundisha shule za
sekondari.
“Baada ya hatua ya kuwaondoa wanafunzi chuoni kuchukuliwa, serikali
ilifanya uchambuzi wa wanafunzi hao kwa lengo la kujiridhisha na sifa
zao. Sifa zilizotakiwa ni ufaulu wa daraja la 1 hadi daraja la 3 na
krediti mbili au zaidi katika masomo ya Sayansi na Hisabati,
“Lakini baada ya uchambuzi kufanyika kati ya wanafunzi wanaosomea ualimu
wa sekondari 6,595 ni wanafunzi 382 pekee ndiyo wana sifa za kuendelea
na masomo yao, 134 ni mwaka wa kwanza na 248 ni mwaka wa pili,” alisema
Prof. Ndalichako.
Aidha alisema kuwa wengine 4,586 wa mwaka wa kwanza wa programu maalum
wa stashahada ya ualimu wa sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu
watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya serikali ambavyo ni Morogoro,
Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo na wanafunzi
1,337 wa mwaka wa pili watahamishiwa vyuo vya Korogwe na Kasulu ili
kumalizia masomo yao.
Pia alisema kuwa serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi
watakaoendelea kusoma UDOM na watarejea chuoni mwezi Oktoba mwaka huu,
huku wale wa vyuo vya ualimu watakuwa wakilipiwa ada ya 600,000 kwa
mwaka ambayo ndiyo ada ya vyuo hivyo na wataripoti chuoni mwezi
Septemba.
Kwa upande wa wanafunzi wa kufundisha elimu ya shule ya msingi, Prof.
Ndalichako alisema wanafunzi 29 wa mwaka wa pili ambao wana cheti cha
daraja A la ualimu watahamishiwa Chuo cha Ualimu Kasulu ili wamalize
masomo yao ila tu kwa gharama zao huku wengine 1,181 akiwataka waombe
nafasi katika vyuo vingine katika masomo ambayo wana sifa zinazolingana
nao.
Aidha katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alisema kuwa migomo
iliyokuwa ikitokea chuoni UDOM kwa walimu kugoma kuwafundisha wanafunzi
hao yawezekana ilikuwa ikichangiwa na wanafunzi hao kwani uwezo wa chuo
cha UDOM ilikuwa ni kupokea wanafunzi 1,180 lakini wakapokea wanafunzi
7,805.
“Walimu kwao mzigo ulikuwa ni mzito wewe utafanya nini?, kwahiyo
tukubali kuwa wingi wa wanafunzi ulichangia kutokea mgomo sababu walimu
wameajiriwa kufundisha na wengine wa digrii sasa kupokea wanafunzi 7,805
na ilitakiwa 1,180 walikuwa wengi,” alisema Prof. Ndalichako.
Tuesday, July 19, 2016
Home
Unlabelled
KATI YA WANAFUNZI 7805 WALIOFUKUZWA UDOM 382 TU NDIO WENYE SIFA
No comments:
Post a Comment