• NEWS & SPORTS

    TANZANIA MPYA

    Sunday, December 11, 2016

    SH291 MIL ZATAFUNWA KUPITIA UJENZI WA VYOO HEWA

     



    SERIKALI mkoani Kilimanjaro, imeshuhudia madudu katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo baada ya halmashauri hiyo kubadili matumizi ya fedha za wafadhili zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kuzitumia kujenga vyoo ambapo pia ilibainika hakuna ujenzi wa vyoo uliofanyika.

    Wilaya hiyo ilipata ufadhili wa Sh milioni 291 kutoka Benki ya Dunia na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa(Tanapa) kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo vya walimu na vya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari wilayani humo.

    Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Mecki Sadiki alitoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hizo na kubaini hakuna vyoo vilivyojengwa licha ya kuwapo taarifa za maandishi zinazoonesha ujenzi huo umekamilika.

    Alisema kati ya fedha hizo Sh milioni 291, kiasi cha Sh milioni 273 kilitolewa na Benki ya Dunia mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya sekta ya elimu huku Sh milioni 18 ilitolewa na Tanapa kwa ajili ya sekta hiyo vile vile.

    Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa huo aliagiza kurejeshwa mara moja kwa fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kazi iliyokuwa imekusudiwa zinazodaiwa kubadilishwa matumizi na Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kutakiwa kutumika kwa ujenzi wa miradi ya elimu kama ilivyokusudiwa.

    Alisema kwa mujibu wa utaratibu, Baraza la Madiwani halipaswi kubadili matumizi ya fedha za wafadhili na za ruzuku kwani fedha hizo huja na maelekezo na masharti yake.

    “Nani aliruhusu kubadilishwa kwa matumizi ya fedha hizi, na hivyo vyoo mnavyodai kujengwa viko wapi…kati ya fedha hizi, Sh milioni 126 nilikwenda mwenyewe kuzichukua Tanapa Arusha ikiwa ni Sh milioni 18 kwa kila halmashauri mkoani hapa kwa ajili ya ununuzi wa madawati,” alisema Sadiki.

    Alisema fedha hizo zilitakiwa kununua madawati lakini kwa wilaya ambazo hazikuwa na upungufu wa madawati, zilipaswa kuelekezwa katika matumizi mengine kwa kumshirikisha yeye jambo ambalo halikufanyika na kumtia mashaka.

    “Kimsingi kama fedha hizi zingetumika kwa ajili ya ujenzi wa vyoo kama mnavyonieleza nisingekuwa na mashaka lakini hivyo vyoo viko wapi….sasa naagiza fedha hizo zirejeshwe mara moja ili ziweze kutumika kwa ajili ya miradi mingine iliyokusudiwa,” alisema.

    Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Monica Mjengi ambaye alikiri kutokujengwa kwa vyoo hivyo kama taarifa yao inavyoeleza huku pia akishindwa kujibu iwapo fedha zilizotengwa kama zimetumika zote katika sekta ya elimu ama la.

    “Mkuu kikweli ni kwamba hakuna choo kilichojengwa kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo,” alisema.

    Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Agness Hokororo alikiri taarifa za kutojengwa kwa vyoo hivyo.

    Hatua hiyo ilimlazimu mkuu wa mkoa kumuagiza mkuu huyo wa wilaya kwa kushirikiana na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Magreth John kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa na kutumika kulingana na maelekezo stahili.HABARILEO

    No comments: