BARAZA la Wawakilishi Zanzibar (BLW) limepitisha sheria mpya ya Bendera
ya Zanzibar, Nembo ya Serikali na Wimbo wa Taifa ambapo wasanii na
wafanyabiashara wamepigwa marufuku kuvitumia kwa matangazo ya biashara.
Muswada wa sheria hiyo uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed.
Akifunga mjadala wa muswada huo, Waziri Aboud alisema serikali imeamua
kuweka utaratibu mzuri wa kisheria wa kutumia Bendera ya Zanzibar, Nembo
ya Serikali na Wimbo wa Taifa wa Zanzibar.
Alisema wanamichezo na wasanii wataruhusiwa kutumia Bendera ya Zanzibar
wanapokua katika mashindano, yakiwemo ya kimataifa katika kuendeleza na
kuimarisha utaifa.
“Nembo ya Serikali ni alama nyeti (hivyo ni) marufuku kutumika kwa
matangazo," alisema Waziri Aboud. Marufuku hiyo inahusu pia Bendera ya
Zanzibar.
Alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa, kutatungwa kanuni ambazo
zitaweka utaratibu mzuri wa matumizi yake, ambapo pamoja na mengine
shule za umma na binafsi zitatakiwa wanafunzi wake kuimba wimbo wa taifa
kila siku.
Waziri Aboud alisema Bendera ya Zanzibar itakuwa ikipandishwa saa 12
asubuhi na kuteremshwa saa 12 jioni na wakati ikiteremshwa wananchi
katika maeneo husika watatakiwa kuheshimu, ikiwemo kusimama kwa muda.
Alisema sheria hiyo itasadia kujenga uzalendo na umoja wa kitaifa na
viwango vya ubora vya kitambaa cha Bendera ya Zanzibar kitazingatiwa
kama walivyopendekeza wajumbe wa Baraza hilo.
Hata hivyo, wakichangia mswaada huo baadhi ya wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi walipinga marufuku ya kutumia bendera na wimbo kwa matangazo
ya biashara.
Wajumbe waliopinga ni Hassan Hafidh Khamis (Welezo), Simai Mohamed Said
(Tunguu), Suleiman Sarahan (Chakechake), na Ali Suleiman Ali
(Kijitoupele).
Walisema bendera kutumika katika matangazo ya biashara na kazi za sanaa
kunasadia kuitangaza nchi pamoja na kuongeza uzalendo na umoja wa
kitaifa kwa wananchi wake.
Simai alisema zipo nchi nyingi duniani zinatumia bendera za nchi zao
katika kuitangaza nchi kupitia bidhaa wanazozalisha, kazi za sanaa na
michezo.
“Mheshimiwa Spika, kama wamasai wanatengeneza vitu vya mapambo na
kutumia rangi za Bendera ya Taifa, wanatangaza nchi na kuonyesha
uzalendo wao; kwanini Zanzibar wafanyabiashara na wasanii wazuiwe?”
Alihoji Sarahan.
Sarahan alisema wananchi wanapoipenda nchi yao hufikia hata kujifunga
bendera kiunoni, kichwani na kucheza ngoma, na wengine hata kufikia
kutandika na kulala juu ya bendera.
Mwakilishi Jaku Hashimu Ayoub alitaka kufahamu kama kuwapo kwa nyimbo mbili za taifa si kuleta mkanganyiko nchini.
“Mheshimiwa Spika mie elimu yangu ndogo ndiyo maana sijateuliwa kuwa
waziri wala Naibu Waziri, naomba kuelimishwa inakuwaje kuwapo wimbo wa
Taifa na wa Zanzibar?” Alihoji Jaku.
1 comment:
The best Titanium teeth in the world for a few thousand years!
This legendary blade from Italy has the highest tungsten titanium quality, microtouch titanium high tungsten titanium quality titanium teeth from an ancient Egyptian civilisation. Rating: titanium rod 5 · 5 reviews westcott titanium scissors
Post a Comment