Mtoto Happiness John Mkazi
wa Seliani Arusha aliyefanyiwa upasuaji kwenye moyo na kupandikiziwa
kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker), ameanza
mazoezi.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto, Sulender Kuboja
aliyeshiriki upasuaji huyo alisema jana kuwa hali ya mtoto huyo
inaendelea vizuri na wameanza kumfanyia mazoezi mepesi.
Dk Kuboja
alisema kwa kawaida mgonjwa yeyote aliyefanyiwa upasuaji anapaswa
kufanyiwa mazoezi mepesi na kwamba kwa mtoto, mazoezi anayofanyiwa ni ya
kukaa, kusimama na kutembea kidogo.
“Hali yake inaonekana kuendelea
vizuri sana... nimetoka kumfanyia vipimo muda mfupi uliopita kifaa kile
kinafanya kazi vizuri na maendeleo yake yanaridhisha sana,” alisema Dk
Kuboja.
Alisema mtoto huyo anaweza kuongea na hata kula chaku- la, hali
aliyosema inaonyesha nafuu nzuri kwake.
Mama mzazi wa mtoto huyo,
Elitruda Malley alisema anaridhishwa na maendeleo ya
afya ya mwanaye kwa kuwa tangu afanyiwe upasuaji huo juzi, hali yake
imeonekana kuimarika kwa haraka.
Mama huyo alisema tangu awekewe kifaa
hicho, mwanaye amekuwa mchangamfu, hali aliyosema inamtia moyo na kumpa
matumaini makubwa.
“Ingawa yupo kwenye oxygen, lakini namshukuru Mungu
kwani anaonekana anapata nafuu nzuri, anatabasamu na kuongea vizuri
kabisa na ana furaha sana, shauku yake ni apone ili aende shule kama
watoto wengine,” alisema Malley.
Aliongeza kuwa mtoto huyo amekuwa
akila vizuri na kumpa moyo kwani mwili wake unaonekana kuwa na nguvu na
afya nzuri.
“Madaktari wapo karibu wakifuatilia afya ya mtoto kwa
ukaribu, wanampa chakula, wanamfanyia mazoezi ya kukaa na kushuka chini,
anaonekana kuwa na nguvu na mwenye maendeleo mazuri. "
Alisema jambo
linalompa faraja ni kuona jinsi madaktari wote wanaomuhudumia mtoto huyo
wanavyofanya kazi hiyo kwa upendo na bidii.
Juzi, kwa mara ya kwanza
katika historia ya Tanzania, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
ilifanikiwa kumpandikiza mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitano kifaa
cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (pacemaker) kinachoendeshwa kwa
betri.
Hayo ni mafanikio ya pili kwa taasisi hiyo ya kisasa ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati baada ya Mei 24 na 25, mwaka huu kufanikisha
operesheni kwa wagonjwa 18 bila kuusimamisha moyo.
No comments:
Post a Comment