WATUMISHI wawili wa Mamlaka ya Mapato
nchini (TRA), wamekamatwa katika operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya
Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kusaidia kupitisha kemikali
bashirifu za ephedrine zinazotumika kutengenezea dawa za kulevya aina ya
heroine.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi
za Mamlaka hiyo zilizoko Upanga, Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni
hiyo, Mihayo Msikhela, alisema pamoja na hao, wapo watumishi wengine
wawili wa TRA ambao nyendo zao zinafuatiliwa.
“Wakati wa
kukabidhiwa majina ya watu wanaojihusisha na dawa hizo nilitamka kuwa
wapo watumishi wa umma wanaosaidia kuingiza hasa kemikali bashirifu,”
alisema.
Kuhusu watumishi hao waliokamatwa ambao hata hivyo
hakuwa tayari kuwataja kwa majina, alisema taratibu zinafanyika na
wakati wowote watafikishwa mahakamani.
Kamishna Msikhela
alisema tayari operesheni hiyo inayofanyika mikoa mbalimbali ya Tanzania
bara kwa kukamata wasambazaji, wauzaji, watumiaji na kuharibu dawa za
kulevya zilizoko mashambani, imeonyesha mafanikio ndani ya siku nne za
mwanzo.
“Dawa za kulevya ziko katika makundi mawili, kundi la
kwanza ni dawa za kulevya zilizoko mashambani na kundi la pili ni dawa
za kulevya za viwandani. Na dawa za kulevya za mashambani kwa kiwango
kikubwa ndio kero iliyopo kwa wananchi wetu. Matokeo haya ni operesheni
ya siku nne tu hadi jana (Alhamisi),” alisema Kamishna Msikhela.
Alisema Mkoa wa Simiyu umeongoza kwa kuteketeza ekari 40 za bangi
ukifuatiwa na Mkoa wa Kipolisi Tarime na Rorya kwa ekari 36 huku Lindi
ukiongoza kwa kukamata dawa za viwandani aina ya heroine ambazo ni kete
50.
Kamishna Msikhela alitaja mikoa mingine iliyofanya vyema
katika operesheni hiyo kuwa ni Tanga ambayo ilikamata mirungi kg 44,
bangi puli 3, Morogoro (bangi kg 18, heroine kete 3), Shinyanga (bangi
kg 10 na gramu 136), Kagera (bangi ekari 14, mirungi ekari 1), Njombe
(bangi nusu ekari na gramu 20), Songwe (heroine kete 274, mirungi kg 3),
Tabora (bangi kilo 6, mbegu kg 18), Singida (bangi misokoto 203,
heroine kete 1), Rukwa (bangi kete 105), Mbeya (bangi kg 5), Kigoma
bangi nusu ekari na Ruvuma bangi gramu 300.
Kamishna huyo
alisema watuhumiwa hao ni wengi na wanaendelea kuhojiwa ambapo baadaye
utafanyika utaratibu wa kisheria kuwafikisha mahakamani.
“Kama
tutaendelea na mlipuko huu ambao umeongezewa mafuta, nina uhakika dawa
za kulevya mashambani zinaweza kupungua kwa kiwango kikubwa. Tuunganishe
nguvu na kuhakikisha vita hii inapiganwa kila sehemu,” alisema Kamishna
Msikhela.
Akijibu swali la waandishi kuhusu kutaja na
kushughulikia majina 97 wakiwemo wanaodaiwa kuwa ni vigogo na watoto wa
vigogo, Kamishna Msikhela alisema kila aliyetajwa ataguswa.
“Yeyote aliyetajwa kwenye orodha hiyo ambayo ni orodha yenye fumbo
ataguswa, hatutazami kwamba kigogo ni yupi na yupi si kigogo, yaliyomo
mle ni majina ya wahalifu kama wahalifu wengine,” alisema Kamishna
Msikhela.
Alisema orodha hiyo ambayo haina muda mrefu tangu ikabidhiwe kwao, ufuatiliaji umeanza na hivyo atatoa taarifa.
Akijibu swali lingine kuhusu orodha za awali zilizowataja kwa majina
watuhumiwa huku ile ya majina 97 wakifichwa, Kamishna Msikhela alisema
ni mfumo unaotumika.
“Ni mfumo uliotumika, yapo makosa ya
mtaani hayaendelei kusumbua tena. Yapo makosa yaliyo wazi na yapo makosa
yaliyojificha. Kwa hiyo yaliyo wazi tutajua yalikuwa katika hatua ipi
na yaliyojificha yako kwenye hatua ipi na yanafanywa vipi,” alisema
Kamishna Msikhela.
Kamishna Msikhela alisema:
“Vita ina
mifumo mbalimbali ya upiganwaji, kwa hiyo mifumo yote itatumika ilimradi
itakupelekea kwenye mafanikio na ukatoka umetangazwa you’re a hero
(shujaa) yote huwa inatumika.”
Alisema vita ya dawa za kulevya
ilianza miaka ya nyuma na kinachofanyika hivi sasa ni mwendelezo kama
ilivyo upambanaji duniani kote.
“Huu ni mwendelezo kama ilivyo
dunia nzima inavyopiganwa na sisi tunawajibika kupigana hii vita mpaka
dunia itakapoweza kuipunguza kabisa au kuimaliza,” alisema Kamishna
Msikhela.
Kamishna Msikhela alisema pamoja na Mamlaka hiyo
iliyotangazwa hivi karibuni, lakini pia kuna vyombo vya ulinzi na
usalama na hasa Jeshi la Polisi ambavyo utaratibu wa kuripoti na kufanya
majukumu yake uko pale pale.
Saturday, February 18, 2017
Home
Unlabelled
WATUMISHI WA TRA WASAIDIA KUPITISHA EPHEDRINE ZA KUTENGENEZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROINE
No comments:
Post a Comment