SERIKALI imetangaza mwongozo mpya kuwa kuanzia sasa masomo ya sayansi ni
lazima kusomwa na wanafunzi wote wanaosoma elimu ya sekondari kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha nne.
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu iliyopo, wanafunzi wanaosoma elimu ya
sekondari wanaweza kuchagua aina ya masomo watakayo wafikapo kidato cha
tatu na kuacha mengine.
Uamuzi huo ulitangazwa jana mjini Tanga na Waziri wa Elimu, Teknolojia,
Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati
akizungumza na mamia ya walimu wa elimu ya msingi kwenye mafunzo ya muda
mfupi kuhusu mtaala mpya wa kufundishia wanafunzi wa darasa la tatu na
nne.
Alisema hivi sasa nchi imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati ambao
ni wa viwanda, hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa kwa sababu ni
wakati sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi watakaoweza
kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini.
Alisema kutokana na uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini kwenye maeneo
mengi, wizara imeamua kuanzia sasa wanafunzi wote wa elimu ya sekondari
kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, watalazimika kusoma masomo ya
sayansi na kufanya mtihani wa masomo hayo, na kwamba baada ya matokeo
kutoka ndipo watafanya uamuzi ama wa kuendelea nayo au la.
Hatua hii kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, itamlazimisha mwanafunzi
kusoma kwa bidii ili kuhakikisha anafaulu masomo hayo ingawa hivi sasa
wanafunzi walio wengi wanadai masomo hayo ni magumu, ndiyo maana
wanachagua kusoma masomo ya sanaa.
Alisema ili kuhakikisha azma ya serikali ya wanafunzi wanapata vitendea
kazi vya masomo hayo, Sh bilioni 12 zimetengwa kwenye bajeti ya fedha ya
mwaka huu kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwenye shule zote za
sekondari nchini ili kuwepo na zana za kufundishia kwa ajili ya masomo
ya sayansi.
"Mafunzo ya vitendo sasa sio mbadala ni lazima, na yatafanywa kama
sehemu ya masomo na wanafunzi wote watalazimika kuyafanya kwa vitendo
ili wawe na uelewa wa walichosoma kwa manufaa ya taifa,” alisema Profesa
Ndalichako.
Alisema Serikali ya Awamu ya tano imedhamiria kuona kiwango cha elimu
kinachotolewa nchini kina hadhi sawa na elimu itolewayo na mataifa
mengine ili kupata wataalamu wenye sifa zinazokidhi mahitaji ya soko
hata kama sio wote wataajiriwa ila hata wale wasiopata ajira wajiajiri
kupitia elimu waliyopata.
Aliwataka walimu waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia uwezo
wao na elimu waliyopata kufanya kazi kwa mujibu wa maadili ya taaluma ya
ualimu ili kuwajengea msingi mzuri wa elimu wanafunzi wa shule za
msingi.
Akizungumzia kauli ya Profesa Ndalichako, Mwenyekiti wa Wamiliki wa
Shule Binafsi Tanzania (TAMANGOSCO), Mahmoud Mringo alisema ni uamuzi
mzuri ila umekuja kwa kuchelewa kwa sababu mahitaji ya wataalamu wa
sayansi nchini ni makubwa kuliko idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo
hayo.
Alisema pamoja na uamuzi huo mzuri uliochukuliwa na serikali, lakini
bado kutakuwa na changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo hayo, maabara
na maktaba na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha mahitaji ya walimu
hao kutoka nje yakaongezeka.
Katibu wa Tamangosco, Benjamin Mkonya alisema ni hatua nzuri ingawa
utekelezaji wake utakuwa na changamoto nyingi kwa sababu hali halisi ya
mazingira ilivyo nchini.
Alisema ikiwa serikali inadhamiria kutekeleza azma hiyo ni vyema
kipengele cha vigezo vya shule kuwepo ambavyo vimeainishwa ndani ya
sheria ya elimu nchini, vikaangaliwa ambavyo ni uwepo wa maabara ya
kutosha, maktaba yenye vifaa na walimu wa kutosha.
Alisema iwapo vigezo hivyo vikiangaliwa shule ambazo hazijakidhi vigezo
hivyo zikafutwa na vifaa vilivyopo kwenye maabara na maktaba hizo
zikaongezwa kwenye shule zenye vifaa hivyo ili kusaidia utekelezaji wa
azma hiyo ya kufundisha masomo ya sayansi kwa wanafunzi wote kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha nne.
Walimu washiriki wameishukuru serikali kwa mafunzo hayo ambayo walisema
ni mazuri na yameongeza kiwango chao cha uelewa na kuwaongezea mbinu za
ufundishaji sambamba na kukuza morali ya kazi zao.
Pamoja na kushukuru, wameomba wizara hiyo iangalie jinsi ya kuweka posho
kwa baadhi ya maeneo ya kazi, hususan kwenye vituo vya kazi vilivyopo
pembezoni na kwenye mazingira magumu ili kuwajengea walimu motisha wa
kufundisha maeneo hayo.
Walimu waliohudhuria mafunzo hayo ni 480 wanaotoka halmashauri za Bumbuli, Mji wa Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Sunday, August 7, 2016
Home
Unlabelled
SERIKALI imetangaza mwongozo mpya kuwa kuanzia sasa masomo ya sayansi ni lazima kusomwa na wanafunzi wote wanaosoma elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
No comments:
Post a Comment